Revelation of John 6

Mwana-Kondoo Avunja Lakiri Saba

1 aKisha nikaangalia wakati Mwana-Kondoo akivunja ile lakiri ya kwanza miongoni mwa zile saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” 2 bNikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda.

3 cAlipoivunja ile lakiri ya pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” 4 dNdipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.

5 eMwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu alikuwepo farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. 6 fNdipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja
Ni kama lita moja.
cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja,
Sawa na dinari moja.
na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”

7 iAlipovunja ile lakiri ya nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” 8 jNikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu
Kuzimu linalotokana na neno Hades la Kiyunani au Sheol kwa Kiebrania.
alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

9 lMwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. 10 mWakalia kwa sauti kuu, wakisema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi juu ya watu waishio duniani kwa ajili ya damu yetu?” 11 nKisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, mpaka idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.

12 oNikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 pNyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 qAnga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

15 rNdipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16 sWakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17 tKwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”
Copyright information for SwhKC